GAVANA WA POKOT MAGHARIBI AMPONGEZA SPIKA WA POKOT BAADA YA KUCHAGULIWA.


Gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin amempongeza spika wa bunge la kaunti hii Fredrick Kaptui kwa kuchaguliwa kama spika wa tatu kuongoza bunge hilo akielezea imani yake kwamba ana uwezo mkubwa wa kuliongoza bunge hilo inavyostahili.
Akizungumza na kituo hiki Kachapin aidha ametumia fursa hiyo kuwataka wabunge katika bunge hilo kutekeleza majukumu yao inavyostahili ikiwemo kutunga sheria za kuwanufaisha wananchi na kuhakikisha kwamba serikali inawajibishwa kando na kuhakikisha ushirikiano mwema miongoni mwao licha ya mirengo ya kisiasa.
Kuhusu mwakilishi wadi anayewakilisha jamii ya wachache katika kaunti hii Kachapin amesema kwamba wataiandikia tume ya uchaguzi IEBC kulalamikia hatua hiyo akisema kwamba kama chama wangependa nafasi hiyo kupewa mkazi wa kaunti hii ambaye anaelewa maswala yanayowaathiri watu hao.
kizaazaa kiliibuka jana katika bunge la kaunti baada ya mmoja wa waakilishi maalum kwa jina Ahmed Desi aliyeteuliwa kupitia chama cha UDA kuwakilisha jamii za watu wachache katika kaunti hii kuondolewa nje ya bunge hilo kufuatia maandamano ya wakazi waliotaka azuiwe kuapishwa.
Kulingana na wakazi waliojawa na ghadhabu nje ya bunge hilo wakiongozwa na timothy Yaoya kutoka jamii ndogo ya Sengwer, uteuzi huo haukupasa kwenda nje ya jamii ya Sengwer kwani ni jamii ambayo inajulikana kuwa jamii ndogo na ina mchango mkubwa kwenye chaguzi za kaunti hii ya Pokot magharibi.
Hata hivyo mwakilishi wadi ya kapchok Peter Lokor amewasuta vikali walalamishi hao akisema walifaa kufuata njia za kisheria kulalamikia hatua hiyo badala ya kuzua kizaazaa akiwataka kusalia watulivu wakisubiri uamuzi wa mahakama kuhusu swala hilo.

WhatsApp us