GAVANA WA POKOT MAGHARIBI AMEAHIDI KUWAONDOA WAFANYAKAZI HEWA

Gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin amekariri kuwa serikali yake itafanya ukaguzi wa kina ili kuwaondoa wafanyikazi wote hewa anaodai kuwa wamechangia kupotea fedha za serikali ambazo zingetumika kutekeleza maendeleo kwa ajili ya wakazi.

Akizungumza baada ya kutangaza rasmi baraza lake la mawaziri, Kachapin amesema kuwa serikali yake imejitolea kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma bora kutoka kwa serikali yake na kwamba kila anayepokea mshahara ni lazima awe anatekeleza majukumu yake inavyostahili.

Kachapin aidha amesema kuwa serikali yake kamwe haitakubali kuendelezwa visa vya ufisadi na watu wachache wenye nia mbovu akionya kuwa yeyote atakayepatikana akiendeleza uovu huo atakabiliwa vikali kisheria ili kuhakikisha fedha zinazopatikana zinaelekezwa kwa kazi inayokusudiwa.

Wakati uo huo Kachapin ameusuta vikali uongozi uliotangulia kwa jinsi ulivyoshughulikia majanga katika kaunti hii akidai kuwa ulielekeza kwingine vifaa vilivyonuia kuwasaidia waathiriwa wa maporomoko ya ardhi miaka mitatu iliyopita na kuwatelekeza pakubwa.