GAVANA WA POKOT MAGHARIBI AHIDI KUTEKELEZA ALIYOSEMA WAKATI WA KAMPEINI
Gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin amewahakikishia wakazi wa kaunti hii kwamba uongozi wake utahakikisha kwamba unatimiza yote aliyowaahidi wakazi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa agosti 9.
Akizungumza baada ya shughuli ya uapisho wa mawaziri alioteua kuhudumu katika baraza lake la mawaziri, Kachapin amewataka wakazi kuwa na subra na kumpa nafasi ya kubuni serikali yake na kisha kuangazia bajeti ya ziada ili kuwa katika nafasi bora ya kutekeleza yote aliyoahidi.
Aidha Kachapin amewapongeza viongozi wa kidini katika kaunti hii kwa ushirikiano ambao wameonyesha akiahidi kushirikiana kikamilifu na viongozi hao kutoka dini zote zinazopatikana katika kaunti hii ya Pokot magharibi katika utendakazi wake.
Wakati uo huo Kachapin amesema kuwa atatoa mazingira bora kwa maafisa wa serikali yake katika juhudi za kuhakikisha kwamba wakazi wa kaunti hii wanapokea huduma bora kutoka kwa serikali yake.