GAVANA LONYANG’APUO ALAANI VIKALI KUFURUSHWA KWA WAKAAZI WA CHEPCHOINA


Gavana wa kaunti hii ya Pokot Magharibi John lonyangapuo ameshutumu mbinu iliyotumika kuwafurusha wakazi kutoka ardhi yenye utata ya Chepchoina mpakani pa kaunti hii ya Pokot Magharibi na ya Trans Nzoia.
Akizungumza eneo la Katikomor alipokutana na wakaazi waliofurushwa katika ardhi hiyo akiwa ameandamana na kamishina wa kaunti hii Apollo Okello na maafisa wengine wa usalama kaunti hii, Lonyangapuo amesema pangeandaliwa mazungumzo kabla ya hatua zozote kuchukuliwa dhidi ya wakazi hao.
Aidha Lonyangapuo ametaka kukamatwa na kuchukuliwa hatua mtu anayedaiwa kuchochea migogoro katika ardhi hiyo kwa kukusanya fedha za wakazi kwa madai ya kuwauzia ardhi.
Wakati uo huo Lonyangapuo ametoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuishi kwa amani na kutowasikiliza viongozi walio na nia ya kuwachochea.
Ni kauli ambayo imesisitizwa na kamishina wa kaunti hii Apollo Okelo ambaye pia amewahakikishia wakazi hao kuwa serikali itayashughulikia malalamishi yao.