GAVANA LONYANGAPUO AIMARISHA SERKALI YAKE KATIKA KUAJIRI MAAFISA ZAIDI

Siku chache baada ya baadhi ya viongozi kaunti hii ya Pokot magharibi kutaja serikali ya gavana John Lonyangapuo kuwa isiyo na maafisa wenye ujuzi katika sekta mbali mbali hali ambayo imepelekea utendakazi duni, gavana Lonyangapuo ameelezea kuwepo na maafisa wenye utaalam wa kutosha.
Katika kikao na wanahabari baada ya kutangaza kuwaajiri maafisa mbali mbali na kuwapandisha vyeo baadhi ambao tayari wanahudumu, gavana Lonyangapuo amesema kuwa serikali yake ni baadhi ya serikali nchini ambazo zina wataalam wa kutosha katika utendakazi wa serikali za magatuzi.

Aidha Lonyangapuo amesema hatua ya kuwaajiri maafisa zaidi na kuwapandisha wengine vyeo haihusiani kwa vyovyote na siasa za uchaguzi mkuu wa mwezi agosti, akisema kuwa hatua hiyo ni moja ya mikakati ya kuimarisha utendakazi wake katika kipindi kilichosalia.

Wakati uo huo Lonyangapuo ametangaza kuwekeza zaidi katika ufadhili wa elimu, uongozi wa kitaalam katika sekta za afya, kilimo, maji na madini katika serikali ijayo iwapo atachaguliwa tena kuongoza kaunti hii kwa muhula wa pili baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi agosti.