GAVANA KACHAPIN ATISHIA KUFUNGULIA MASHITAKA SERIKALI YA UINGEREZA KUFUATIA MAUAJI YA KOLOWA.


Gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin amekariri msimamo wake wa kufungua kesi dhidi ya serikali ya uingereza kufuatia mauaji ya wafuasi wa dini ya mafuta pole yanayodaiwa kutekelezwa eneo la kolowa na serikali ya taifa hilo.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya kila mwaka ya dini hiyo eneo la Tamugh katika wadi ya Sook, Kachapin alisema kwamba wafuasi wengi wa dini hiyo waliuliwa bila hatia na utawala wa kikoloni na sasa ni wakati wanafaa kupata haki.
Alisema kwamba atatumia fursa yake kama gavana wa kaunti hii kuhakikisha kwamba waathiriwa wote wa unyama huo wanafidiwa.
“Nitaanzisha kesi na watu wa uingereza kwa kuwa waliwaua watu wetu hapa bila ya hatia yoyote. Nataka familia za watu waliouawa na wakoloni huko kolowa wapate haki. Vile nimekuwa gavana sasa niko katika nafasi bora ya kufanya hivyo.” Alisema Kachapin.
Aidha Kachapin alisema kwamba hatua ya serikali kuthibitisha kwamba wafuasi wa dini hiyo waliouliwa hawakuwa na hatia yoyote inatoa fursa mwafaka kwake kuiwajibisha serikali ya uingereza kwa uovu waliotendewa wafuasi hao.
“Hali kwamba serikali ya Kenya imekubali kwamba watu wetu waliopitia mahangaiko hayo hawakuwa na hatia yoyote, ila waliuawa wakiabudu, inanipa fursa bora ya kuifungulia serikali ya uingereza mashitaka.” Alisema.