GAVANA KACHAPIN ATETEA TEUZI ZA RAIS RUTO ZA MAKATIBU WAKUU WA UTAWALA.

Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ametofautiana na viongozi ambao wanamkosoa rais William Ruto kufuatia uteuzi wa makatibu wa utawala kwa madai ya kuongeza mzigo kwa mlipa ushuru wakati ambapo taifa linakabiliwa na hali ngumu ya uchumi.

Akizungumza katika mahojiano na kituo hiki Kachapin alisema ni jukumu la serikali kuwapa wananchi wake nafasi za ajira akisistiza kwamba uteuzi wowote wa maafisa wa serikali hauwezi kuathiri uchumi wa nchi katika serikali ambayo ina mipangilio bora ya utekelezwaji wa majukumu yake.

“Wakenya ambao wanakosoa teuzi za rais hasa za makatibu wa utawala nadhani hawafahamu kwamba kuajiri watu ni jukumu la serikali. Kuwaajiri watu hakuwezi kwa vyovyote vile kuhujumu uchumi kwa serikali yoyote ambayo ina mipangilio bora ya jinsi ya kutekeleza majukumu yake.” Alisema Kachapin.

Aidha Kachapin alitumia fursa hiyo kumpongeza rais Ruto kwa kuwateua makatibu wa utawala wawili kutoka kaunti ya Pokot magharibi akisema hatua hiyo imewapelekea wakazi kuhisi kujumuishwa katika serikali ikizingatiwa kaunti hiyo ilitengwa kwa miaka mingi na serikali zilizotangulia.

“Namshukuru rais kwa kuwateua makatibu wa utawala wawili kutoka jamii ya Pokot. Hiyo inatufanya sisi pia kuhisi kuwa katika serikali kwa sababu kwa muda mrefu jamii hii haijakuwa na uwakilishi mzuri katika serikali. Tangu kujinyakulia uhuru tumekuwa na mawaziri wawili pekee.” Alisema.

Wakati uo huo Kachapin alisema kwamba rais amejumuisha maeneo yote ya nchi katika teuzi za maafisa wa serikali yake na kwamba wanaokosoa teuzi hizo wanaingiza tu siasa katika maswala yasiyostahili kupigiwa siasa.

“Mimi naona rais amejumuisha maeneo yote ya taifa hili katika teuzi zake, kwa hivyo wale wanaokosoa wanajaribu tu kuingiza siasa kwa kila kitu ambacho rais anafanya.” Alisema.