GAVANA KACHAPIN AMSUTA PKOSING KWA MADAI YA KUTUMIA VYOMBO VYA HABARI KUMHARIBIA SIFA.

Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amemsuta vikali mbunge wa pokot kusini David Pkosing kwa kwa kile alisema kutumia vyombo vya habari kumharibia sifa machoni pa wakazi.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Kachapin amemtaja Pkosing kuwa kiongozi mwenye hasira na majivuno akimtaka kufahamu kwamba yeye ni kiongozi aliye na jukumu la kutimiza ahadi alizotoa kwa wakazi wa eneo bunge lake.

Kachapin alisema kwamba Pkosing amepagawa na ndoto ya kuwa gavana wa tatu wa kaunti hii ya Pokot magharibi, ndoto ambayo kulingana naye ni ya kishamba kuwa nayo wakati huu na dhihirisho la kiongozi asiye na ukomavu.

Alimtaka mbunge huyo kufahamu kwamba yeye ndiye gavana wa kaunti hii na ana idhini ya wakazi waliompigia kura kwa wingi katika uchaguzi mkuu uliopita.

Aidha Kachapin alimshauri Pkosing kuelekeza nguvu zake kwa maswala yanayokusudiwa kuwaunganisha wakazi wa kaunti hii na wala si kuwagawanya.