GAVANA KACHAPIN AMSUTA LONYANGAPUO KWA KUTELEKEZA MIRADI ALIYOANZISHA.

Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amesifia jengo jipya la bunge la kaunti hiyo analosema kwamba litakuwa bunge la kisasa litakalotoa mazingira bora kwa waakilishi wadi kutekeleza shughuli zao kikamilifu bila changamoto.

Akizungumza wakati akikagua jengo hilo, gavana Kachapin aliisuta serikali ya gavana John Lonyangapuo kwa kulitelekeza jengo hilo pamoja na miradi mingine ambayo alianzisha katika awamu yake ya kwanza alipohudumu kama gavana wa kaunti hiyo.

“Bunge ambalo limejengwa ni la kisasa na tunalenga kulikamilisha haraka iwezekanavyo ili wabunge wetu wa kaunti wapate nafasi nzuri ya kutekeleza kazi yao ya kuwawakilisha wananchi. Jengo hili pamoja na miradi mingine lilitelekezewa na gavana aliyekuwa kwa misingi ya kisiasa.” Alisema Kachapin.

Kachapin alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa maafisa wa serikali kutokuwa na mazoea ya kutelekeza miradi ambayo inaanzishwa na watangulizi wao kwani miradi hiyo si ya mtu binafsi bali inanuia kuwanufaisha wananchi kwani inatekelezwa kwa kutumia fedha za umma.

“Ombi langu kwa viongozi ni kwamba ukianzisha miradi ni lazima ikamilishwe, kwa sababu hii ni miradi ya wananchi na ni fedha za umma ambazo zimetumika. Si fedha za mtu binafsi.” Alisema.

Spika wa bunge la kaunti hiyo Fredrick Kaptui ambaye aliandamana na gavana Kachapin katika ukaguzi wa jengo hilo alisema kwamba itachukua muda wa miezi mitatu kabla ya jengo hilo kukamilika akimpongeza gavana kachapin kwa juhudi anazoendeleza kurahisisha shughuli za waakilishi wadi.

“Tunatarajia bunge hili kukamilika kwa muda wa miezi mitatu ijayo. Tunamshukuru gavana kwa ushirikiano ambao ametupa kama bunge kuhakikisha kwamba shughuli zetu za kuwawakilisha wananchi zinarahisishwa.” Alisema Kaptui.