Gavana Kachapin amlaumu seneta Murgor kwa kusimamishwa fedha za basari

Gavana wa kaunti ya Pokot Magharibi Simon Kachapin, Picha/Benson Aswani

Na Benson Aswani,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameendelea kumlaumu seneta wa kaunti hiyo Julius Murgor kwa kile amesema ndiye aliyesababisha kusimamishwa fedha za basari ambazo zimekuwa zikitolewa kwa magavana nchini.


Akizungumza eneo la Bendera, gavana Kachapin alisema hatua ya seneta Murgor kulalamikia katika kikao cha seneti, hatua ya kuzinduliwa basari kabla ya kulipwa walimu wa ECDE, ndiyo iliyopelekea kamati ya elimu katika bunge la seneti kuandikia mdhibiti wa bajeti kusimamisha fedha za basari.


Alisema kwa sasa hamna kaunti ambayo inaruhusiwa kupeana fedha za basari kote nchini kufuatia hatua ya seneta Murgor kuibua swala hilo kwenye kikao hicho cha kamati ya elimu katika seneti, kilichotumiwa kumhoji gavana Kachapin kuhusiana na maswala ya elimu kaunti hiyo.


“Tatizo la basari lilianzia hapa West Pokot. Nilienda seneti, na nilipowaambia kwamba tutalipa walimu wa ECDE januari mwaka huu, wakaniambia kwa nini hujalipa walimu huu muda wote, nikasema bajeti haikutosha. Seneta wenu akasema mbona unapeana basari milioni 600 na hujalipa walimu. Sasa kamati ya elimu ya seneti ikaamua kuandikia mdhibiti wa bajeti kusimamisha basari,” alisema Kachapin


Gavana Kachapin alitumia fursa hiyo kuwahimiza viongozi kuwa makini na maswala ambayo wanazungumza katika vikao muhimu ili wasiweze kusababisha matatizo kama yale ambayo sasa yanashuhudiwa kote nchini kufuatia kosa la mtu mmoja.


“Ndio mimi nawaambia viongozi wenzangu, tujue jinsi tunazungumza katika vikao muhimu kama hivyo. Unaona sasa kaunti zote zinaumia kwa sababu tu ya mtu mmoja,” alisema.


Kachapin aliyasema haya katika hafla ya kuwachangia kina mama fedha za kuandeleza shughuli zao za kibiashara eneo la Bendera, eneo bunge la Kapenguria.