GAVANA KACHAPIN AKAGUA KIWANDA CHA KUCHINJA MIFUGO CHA NASUKUTA ENEO LA POKOT KUSINI
Gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin amewahakikishia wakazi wa kaunti hii kwamba kiwanda cha nyama cha Nasukuta kitaanza rasmi kuhudumu mapema mwaka ujao.
Akizungumza baada kuzuru kiwanda hicho pamoja na naibu gavana Robert Komole na waakilishi kutoka benki ya dunia, Kachapin amesema kuwa kiwanda hicho kitachangia pakubwa ukuaji wa uchumi wa kaunti hii huku akiwataka wahusika wote katika mradi huo kuhakikisha kinaanza kuhudumu haraka iwezekanavyo.
Aidha amesema kuwa atatafuta ushauri kutoka kwa wataalam pamoja na wawekezaji katika soko la mifugo ili kuafikia malengo hitajika ya mradi huo.
Kwa upande wake waziri wa kilimo, unyunyiziaji maji mashamba na mifugo Evans Menach amesema kuwa mradi huo umefikia asilimia 98 na kuwa kitaanza kuhudumu katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Ni kauli ambayo imesisitizwa na mwenyekiti wa bodi ya kichinjio hicho cha Nasukuta Dkt James Merisia ambaye aidha amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuchinja ng’ombe 100 na mbuzi 200 kwa siku moja.