FURAHA YA KUUNGANA NA JAMAA BAADA YA ZAIDI YA MIAKA MIWILI.
Wananchi wametakiwa kuwatunza vyema jamaa zao wenye matatizo ya akili kutokana na changamoto zinazotokana na watu hao katika jamii, na vile vile kufanya mazoea kutumia idara ya polisi kuwasaka iwapo wataweza kutoweka.
Ni wito wake OCS wa kituo cha polisi cha kacheliba katika kaunti hii ya Pokot magharibi Tom Nyanaro aliyekuwa akizungumza baada ya kuunganisha jamii moja kutoka eneo la Chesamisi kaunti ya bungoma na jamaa yao mwenye matatizo ya akili ambaye alitoweka miaka miwili iliyopita kabla ya kupatikana eneo la Kasei katika kaunti hii.
“Nilipata habari kwamba kuna mama alikuwa amejifungua akili yake si nzuri, tukamhoji kidogo akasema jina lake na anakotokota, nikaweka habari hiyo kwa mtandao, na baada ya muda mchache nikapata simu kutoka kwa familia yake.” Amesema Nyanaro.
Muuguzi mkuu katika hospitali ya kacheliba Luke Kanyang’areng amesema kuwa walipokea taarifa kutoka eneo la Kasei kuhusu mwanamke huyo ambapo walifika huko na kumpata akiwa tayari amejifungua mtoto wa kike ambapo walimshughulikia kabla ya kuwasiliana na maafisa wa polisi kuhusu kisa hicho.
“Muuguzi wetu mwenye alikuwa zamu ya usiku alipigiwa simu kwamba kuna mgonjwa kasei. Alipofika pale akamkuta tayari amejifungua. Akamleta pamoja na mtoto wake. Nilipofiak kazini asubuhi nikapa kwamba alikuwa mama mwenye akili taahira.” Amesema.
Aliongeza kwa kusema,”tulihakikisha mama ameoga na amepata matibabu, tukashughulikia mtoto kwa kumpa joto na kuhakikisha kuwa analala mahali pazuri. Ndipo tukawasiliana na OCS.”
Kakake mwanamke huyo Eric Kakai amewapongeza wote waliohusika katika kupatikana kwa dadake hasa kwa Zaidi ya miaka miwili akisema kuwa si mara ya kwanza kwake kutoweka nyumbani kwani aliwahi kufanya hivyo awali.
“Huyu msichana alikuwa amepotea kwa muda wa miaka miwili sasa na nimefurahia sana kwa vile nilipata ripoti kwa mtandao, nikampigia OCS simu ambaye alinipa maelezo na nikaja hadi nikampata mahali yuko.” Alisema.
Faith Tapkar ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya upili ya Chepareria ambaye alilazimika kuishi na mwanamke huyo hadi alipopata msaada.