FAMILIA MOJA KACHELIBA NUSRA ITUMIE MBOLEA KAMA CHAKULA KUFUATIA MAKALI YA NJAA.

Serikali ikiendelea kupeana mbolea ya bei nafuu kwa wakulima maeneo mbali mbali ya nchi, familia moja eneo la Riwo eneo bunge la kacheliba kaunti ya Pokot magharibi nusra ile mbolea hiyo kwa kudhani kuwa ni chakula cha msaada.

Kulingana na wakazi hao, machifu wa eneo hilo waliwaagiza kujisajili katika mpango wa serikali wa kupeana mbolea ya bei nafuu bila kufahamishwa lengo kuu la zoezi hilo la usajili, wao wakidhani kwamba wanafanya hivyo ili kupata msaada wa chakula.

“Hapa sisi hatutumii mbolea. Sasa kuna wale ambao walienda kununua huko Makutano tukafikiria ni chakula. Kumbe ni vitu vyenye haviliki. Tumejaribu kupika tukaona inatoa maji mbaya sana tukashangaa ni chakula gani hiki. Mzee wa kijiji alikuja kutuandika majina hapa sisi tukadhani ni chakula cha msaada kwa sababu hawakutueleza ni kwa nini wanachukua majina yetu.” Alisema mkazi.

Wakazi hao sasa wanatoa wito kwa serikali kuwapa chakula cha msaada badala ya mbolea kwani kwa sasa wanakabiliwa na makali ya njaa, wakisema kwamba mashamba ya eneo hilo yana rutuba ya kutosha na hayahitaji mbolea wakati wa upanzi.

“Badala ya kutuletea mbolea serikali inapasa kutuletea chakula. Tuna njaa sana huku, na sisi mashamba yetu hayategemei mbolea. Yana rutuba ya kutosha.” Alisema.

Afisa katika shirika la Rural women peacelink Rosana Kashiol alitoa wito kwa serikali kubaini mahitaji ya maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo na kutoa mbegu kwa maeneo yasiyohitaji mbolea akielezea hofu huenda familia zaidi zikahatarisha maisha yao kwa kudhani kwamba mbolea inayopeanwa ni chakula cha msaada.

“Karibu huyu mama awalishe watoto wake mbolea akidhani ni chakula. Mimi naomba serikali ikiwezekana itambue kila eneo na mahitaji yake. Kama ni mbolea wapeame sehemu inayohitaji mbolea ila huku wawape watu mbegu kwa sababu sasa watu watakula mbolea wakidhani ni chakula.” Alisema Kashiol.