ENEO LA STATE LODGE KUFUNGULIWA ENEO LA TURKWEL POKOT MAGHARIBI.

Wizara ya usalama nchini kwa ushirikiano na mamlaka ya maendeleo eneo la Kerio Valley KVDA inaendeleza mikakati ya kufufua eneo litakalotumika na rais kuendeleza shughuli zake maarufu state Lodge eneo la Turkwel katika kaunti ya Pokot magharibi.

Akiongoza ujumbe wa rais kuangazia jinsi utakavyotekelezwa mradi huo, katibu katika wizara ya usalama wa ndani ya nchi Raymond Omolo, alisema wanashirikiana na mamlaka ya KVDA na kampuni ya KenGen kuandaa mazingira bora ambayo yatatumika na rais katika shughuli zake anapozuru kaunti hiyo.

“Tumezungumza na mamlaka ya KVDA na kampuni ya KenGen kuhusu kufufua eneo la state lodge huku Turkwel, ambapo rais atakuwa akifanyia shughuli zake akizuru kaunti hii ya Pokot magharibi.” Alisema Omolo.

Gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin alisema kufufuliwa eneo hilo kutakuwa na manufaa makubwa kwa kaunti hiyo kiuchumi, kwani sasa shughuli nyingi za rais zitaendelezwa eneo hilo na hata kuvutia watalii kando na kuhakikisha usalama unaimarishwa.

“Eneo hili likifufuliwa litaimairisha sehemu hii ambayo ilikuwa imerejea chini sana kimaendeleo, kwa sababu uwepo wa rais hapa utaimarisha hali ya usalama na kuvutia watalii, hali ambayo itaimarisha kaunti hii kiuchumi.” Alisema Kachapin.

Mkurugenzi wa KVDA Sammy Naporos alisema mradi huo utakamilika kufikia mwezi desemba mwaka huu akitoa wito wa ushirikiano kutoka kwa wadau mbali mbali ili kuhakikisha kwamba unaharakishwa na kuanza kuwaletea manufaa wakazi.

“Tunaomba ushirikiano kutoka kwa wadau wote ikiwemo wananchi na vitengo vyote ili kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika kufikia mwezi desemba mwaka huu.” Alisema Naporos.

Viongozi kaunti hiyo wamepongeza mradi huo wakisema utachangia katika kuwapa ajira wakazi pamoja na kupunguza safari za viongozi kuelekea jijini Nairobi kukutana na rais kwa ajili ya maendeleo.