DUALE: VIKOSI VYA KDF VITAKITA KAMBI BONDE LA KERIO HADI UHALIFU UMALIZIKE.

Waziri wa ulinzi Aden Duale amesema kuwa maafisa wa kikosi cha ulinzi KDF hawataondolewa kwenye eneo la Kerio valley hadi wahalifu watakapokabiliwa.

Akiongea kwenye ziara yake katika baadhi ya maeneo ya kerio valley, Duale alisema kuwa serikali ya sasa ina nia na mbinu za kuwakabili wahalifu wanaojihusisha na wizi wa mifugo.

Aidha Duale aliwataka wakazi kuendelea kudumisha amani huku akiongeza kuwa serikali ina mipango ya kufanikisha miradi tofauti ya maendeleo katika eneo hilo ikiwamo kuanzisha shule za bweni.

“Liwe liwalo lazima wakazi wa kerio valley wapate amani. Na hakuna mahali sisi kama KDF tunaenda. Na iwapo tutaona hawa watu wanacheza, tutazidisha kambi za jeshi. Serikali zilizotangulia zilishindwa kutatua hali hii, lakini sisi kama serikali ya William Ruto tutahakikisha tunamaliza tatizo hili.” Alisema Duale.

Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin kwa upande wake alitoa wito kwa waziri Duale na mwenzake wa usalama na maswala ya ndani ya nchi Kithure Kindiki kuongeza maafisa wa usalama eneo la Kamologon kama njia moja ya kuhakikisha usalama eneo hilo.

Kachapin alisema miradi ya maendeleo imelemazwa eneo hilo kwa miaka mingi kufuatia harakati za wezi wa mifugo.

“Sisi tunataka tu jinsi ulizungumza nasi, uweke kambi ya jeshi pale Kamologon. Nilijenga hospitali hapo mwaka 2014 lakini haiwahudumii wakazi kufuatia utovu wa usalama.” Alisema Kachapin.

Waziri wa barabara Kipchumba Murkomen alisema kama njia moja ya kuhakikisha usalama eneo la kerio valley, wizara yake kwa ushirikiano na kaunti za bonde la kerio zinaweka mikakati ya kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kwa manufaa ya wakazi wa kaunti hizo.

“Wizara yangu imekubaliana na viongozi wa kaunti za kerio valley kwamba katika muda wa majuma mawili tuweke mipangilio ya jinsi ya kutekeleza miradi mikubwa katika kila kaunti ili kuwafaidi wananchi wa kaunti hizi kama njia moja ya kukabiliana na uhalifu.” Alisema Murkomen