DORIA ZA PAMOJA ZAENDELEZWA MIPAKANI PA POKOT MAGHARIBI NA TURKANA KUHAKIKISHA USALAMA.

Mikakati inaendelea kuwekwa kuhakikisha kwamba usalama unadumishwa mipakani pa kaunti hii ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Turkana.
Kulingana na OCPD wa eneo la Pokot ya kati Bamford Surwa, maafisa wa usalama kutoka pande zote mbili watafanya doria ya pamoja maeneo hayo ili kuhakikisha kuwa wakazi wanalisha mifugo yao bila ya hofu ya kuvamiwa na wezi wa mifugo.
Aidha Surwa amesema kuwa wanaendesha uchunguzi kuhusu visa vya uvamizi akiahidi kuhakikisha kwamba wahusika wanakabiliwa na mkono wa sheria mbali na kurejesha mifugo walioibwa na hawajarejeshwa kufikia sasa.
Wakati uo huo Surwa ametaka kutohusishwa jamii nzima za pande zote mbili na visa hivyo vya wizi wa mifugo, akisema kuwa ni wahalifu wachache wanaotatiza amani na ambao watakabiliwa kulingana na sheria, huku akitoa wito wa ushirikiano kutoka kwa jamii katika kuhakikisha wahalifu hao wanaandamwa.