Deni la serikali ya kaunti lawanyima wakulima Pokot magharibi mbegu kutoka Kenya seed

Simon Kachapin Gavana wa kaunti ya Pokot Magharibi, Picha/Benson Aswani
Na Benson Aswani,
Wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi watalazimika kugharamika zaidi msimu huu wa upanzi baada ya serikali ya kaunti kukiri kwamba haitaweza kutoa mbegu kwa wakulima jinsi ilivyokuwa miaka ya awali.
Akizungumza jumatano afisini mwake, gavana Simon Kachapin alisema hali hii imetokana na hatua ya kampuni ya kuzalisha mbegu ya Kenya seed ambayo imekuwa ikisambaza mbegu kwa kaunti hiyo kuweka sheria mpya kwamba haitasambaza mbegu kwa kaunti yoyote ambayo inadaiwa na kampuni hiyo.
Gavana Kachapin aliilaumu serikali iliyotangulia kwa kuacha deni kubwa la kampuni hiyo, juhudi za serikali yake kuandaa mazungumzo na hata kuchukua hatua za kulipa kiwango fulani ili angalau wakulima katika kaunti hiyo wapewe mbegu na kampuni hiyo zikiambulia patupu.
“Tulipata deni kubwa lililoachwa na serikali iliyopita, na tumejaribu kupunguza deni hilo, lakini kampuni ya Kenya seed ilipitisha sheria mpya kwamba wale ambao hawajamaliza deni hawatapata mbegu. Tumejaribu sana kuongea na wakurugenzi wa kampuni ila wameshikilia kwamba lazima tulipe deni hilo,” alisema Gavana Kachapin.
Gavana Kachapin alisema serikali yake ilikuwa imetenga bajeti ya ununuzi wa mbegu mwaka huu ila sasa kutokana na sheria hiyo mpya ya kampuni, serikali yake haitaweza kununua mbegu kwa wakulima mwaka huu ikizingatiwa msimu wa upanzi unayoyoma.
Aliwataka wakulima kuvumilia gharama ya upanzi mwaka huu akiahidi kwamba serikali yake inajipanga kwa ajili ya mwaka ujao wakati ambapo itakuwa imeshughulikia deni inalodaiwa kwa sasa na kampuni hiyo ya kuzalisha mbegu.
“Tulikuwa tumetenga shilingi milioni 60 mwaka huu za kununua mbegu. Lakini hawa wanataka tulipe kwanza na siku zinaenda. Sasa tutafanya nini? Kwa hivyo tunataka kujipanga kwa ajili ya mwaka ujao tukishalipa deni tunalodaiwa,” alisema.