DARA YA AFYA POKOT MAGHARIBI YAELEZEA WASI WASI KUHUSU ONGEZEKO LA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA HIV MIONGONI MWA VIJANA.

Takwimu zinaonyesha kwamba kuna ongezeko la maambukizi ya virusi vya HIV hasa miongoni mwa vijana katika kaunti ya Pokot magharibi.

Kulingana na mshirikishi wa maswala ya HIV na magonjwa ya zinaa eneo la pokot kaskazini Jacob Rotich, walioathirika zaidi na virusi hivyo ni watu kati ya umri wa miaka 19 hadi 29 hali inayochangiwa pakubwa na hulka ya kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja.

Rotich aidha alisema kwamba wadau katika sekta ya afya kaunti hiyo wanakongamana kwa siku tano kujadili jinsi ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo hasa kutoka kwa mama hadi kwa mtoto wakati wanapojifungua.

“Takwimu ambazo zimeendeshwa hivi karibuni zinaonyesha ongezeko la maambukizi ya virusi vya HIV miongoni mwa vijana kati ya umri wa miaka 19 hadi 29. Hali hii imechangiwa pakubwa na hulka ya vijana kushiriki ngono na mpezi zaidi ya mmoja.” Alisema Rotich.

Rotich alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa vijana kuwa waangalifu na kutumia mbinu za kuzuia maambukizi ya virusi vya HIV, kuu zaidi akishauri haja ya kujizuia na ngono za mara kwa mara kama njia bora ya kuzuia maambukizi ya virusi hivi.

Aidha alitoa wito kwa wananchi kuwa na mazoea ya kutembelea vituo vya afya ili kubaini hali zao kuhusu maambukizi ya HIV.

“Vijana wanapasa kuwa waangalifu na kuhakikisha kwamba wanatumia mbinu za kuzuia maambukizi. Hasa tunashauri vijana kujiepusha na ngono za kiholela kwani hii ndio njia bora ya kuzuia ugonjwa huu. Pia tunawahimiza wananchi kuzuru vituo vya afya ili kubaini hali zao.” Alisema.