CHUO KIKUU CHA ELDORET CHAENDELEZA MRADI WA KUHIFADHI UDONGO NA KUTUNZA MAZINGIRA CHEPARERIA.

Chuo Kikuu Cha Eldoret kupitia kwa Wakfu wa Utunzaji wa Mazingira na uzalishaji kupitia ukulima  kinaendeleza mradi wa kuzuia mmomonyoko wa udongo kwa kujenga vizuizi kwenye mikondo ya maji katika eneo la Chepareria, kaunti ya Pokot Magharibi huku wakulima wakipokezwa miche na vifaa vingine vya kutumika katika kutunza mazingira.

Wakfu huo wa FRM umeongozwa na daktari Wanyama na Ruth Njoroge ambao walitumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa kutunza udongo wakisema lengo lao kuu katika mradi huo ni kuwapa wakazi wa maeneo husika  vifaa vya kuwawezesha  kuendeleza mradi huo.

“Hawa ni wakulima ambao awali walikuwa tu wafugaji ila sasa wanajihusisha na kilimo cha mimea. Lengo kuu la shughuli hii ni kuhifadhi udongo na maji. Tunawapa wakazi hawa vifaa vya kuwasaidia kuhifadhi udongo.” Walisema.

Waziri wa Kilimo katika Kaunti ya Pokot Magharibi Wilfred Lopuonyang na mwenzake wa maji na Mazingira Lucky litole, waliwasihi wakulima kushirikiana kikamilifu na chuo hicho wakisisitiza kwamba wakazi wa Kaunti hiyo wamepewa miche ya kupanda kwa ajili ya kutunza mazingira.

“Nasisitiza sana umuhimu wa kupanda miti. Miti itatusaidia sote kutunza mazingira. Katika idara yetu tumepeana miti kwa wakazi katika kaunti zote ndogo ambapo wamepanda ili kutimiza malengo haya.” Walisema.

Naibu chifu wa Senetwo Mark Lokatang’o aliwashukuru wahisani hao wa chuo kikuu cha Eldoret akisema mradi huo unaendelea kubadilisha hali ya mazingira kutoka kwenye hali mbovu iliyokuwepo awali.

“Mazingira yetu yanaimarika sana ambapo pia mmomonyoko wa udongo umezuiliwa pakubwa. Kwa hivyo mradi huu umekuwa wa manufaa makubwa kwetu sisi.” Alisema Lokatang’o.