CHIFU WA SONGOK ADAI KUWINDWA NA SHIRIKA LA NRT.


Mzozo kati ya wakazi wa kaunti ya Pokot Magharibi na shirika na NRT[Northern Rangelands Trust ] umechukua mkondo mpya huku chifu mmoja wa eneo hilo akidai kuwa maisha yake yamo hatarini na kukashfu maafisa wa shirika hilo kwenye kaunti kwa kuwa na njama ya kumwangamiza.
Naibu wa chifu wa Lokesheni ndogo ya Songok Joseph Korkimul sasa anadai kuwa maafisa wanaohudumu kwenye mbuga ya kuhifadhi wanyama ya Pellow eneo la Turkwel, baadhi ya viongozi wa eneo hilo na maafisa wa serikali wanataka kumuangamiza kutokana na msimamo wake wa kupinga huduma za shirika hilo katika eneo hilo.
Kulingana na chifu huyo,shirika hilo litatumia askari wake wa mbuga na maneja wa mbuga ya wanyama ya Pellow kukatisha maisha yake.
Korkimul amesema kuwa shirika hili linafaa kukomesha shughuli zake eneo hilo akidai linachangia uhasama kati ya jamii.
Anadai kuwa shirika hilo limechora ramani ya mashamba suala wanalosema huenda likachochea uhasama kati ya jamii jirani na kuwa limefeli kuwa na uwazi, kuwajibika na limewatenga na kutoshirikisha wakazi katika shughuli zake.
Hata hivyo uongozi wa shirika hilo la NRT umekanusha vikali madai hayo ukisema shirika hilo lilitafuta eneo ambalo litakuwa likifanyia kazi wala halina lengo la kupokonya wakazi ardhi likitaja madai ya chifu huyo kuwa uongo.
Alisema kuwa mradi wa mbuga umesaidia kuleta amani kati ya jamii za Pokot na Turkana kwa miaka sita sasa kwani vijana wengi wameajiriwa na shirika hilo chifu huyo ni mtu anayetafuta sifa kwani amepoteza umaarufu.