CHANJO ZAIDI DHIDI YA CORONA ZATARAJIWA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI MWEZI HUU WA SEPTEMBA.


Kaunti ya Pokot magharibi inatarajiwa kupokea chanjo mpya dhidi ya virusi vya corona za Pfizer, moderna na Johson and Johnson kando na ile ya astrazeneca ambayo imekuwa ikitumika ili kuendeleza shughuli ya kuwachanja wananchi.
Mkurugenzi katika wizara ya afya kaunti hii Nobert Abuya amesema kuwa chanjo hizo zinatarajiwa kuwasilishwa katika kaunti hii mwezi huu wa septemba baada ya kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya kuhusu jinsi ya kuzihifadhi na kuzitumia.
Abuya amesema kuwa wahudumu wa afya watalazimika kupokea mafunzo kutokana na hali kuwa chanjo hizo zinatofautiana katika mazingira ambayo zinahifadhiwa na kuwa iwapo zitatumika bila kuzingatia kanuni zinazostahili huenda zisiafikie matokeo yanayohitajika.
Amesema mafunzo hayo yatatolewa na maafisa kutoka afisi kuu inayosimamia chanjo nchini, akiwataka wakazi wa kaunti hii kuwa na subra hatua zote zinapofuatwa kabla ya chanjo kuanza kutolewa.