CHANJO DHIDI YA UGONJWA WA UKAMBI KUANZA LEO.


Siku moja tu baada ya wizara ya afya kwa ushirikiano na shirika la kimataifa la kuwashughulikia watoto UNICEF kuzindua rasmi chanjo dhidi ya surua yaani Measles, wizara ya afya kaunti hii ya Pokot Magharibi imaefanya warsha ya siku moja kwa washikadau wote wa afya.
Akizungumza na wanahabari baada ya warsha hiyo, waziri wa afya kaunti hii ya Pokot Magharibi Christine Apakorongí amesema kuwa hatua hiyo imeafikiwa baada ya ugonjwa huo kuripotiwa katika kaunti hii ya Pokot Magharibi mapema mwezi huu.
Watoto zaidi ya milioni 3.5 hata hivyo wanatarajiwa kupokea chanjo hiyo wenye umri wa kati ya miezi 9 na miaka 5.
Shughuli hiyo inatarajiwa kuanza leo kudumu kwa siku 10 katika kaunti hii na kaunti nyingine 22 ambazo zimetambuliwa kuwa kwenye hatari kubwa ya kukumbwa na mlipuko huo ikiwa ni pamoja na Trans Nzoia, Bungoma, Busia, Turkana, Elgeyo Marakwet miongoni mwa nyingine.
Ikumbukwe katibu mkuu katika wizara ya afya Dkt Mercy Mwangangi alisema kuwa Chanjo hiyo ni salama na itatolewa bila malipo kwa watoto zaidi ya milioni 3.5.