CHANJO DHIDI YA SURUA YATARAJIWA KUTOLEWA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI


Idara ya afya katika kaunti hii ya Pokot magharibi inatarajiwa kuanza kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Surua au measles kwa watoto wenye chini ya umri wa miaka mitano kuanzia tarehe 7 mwezi juni.
Haya ni kwa mujibu wa mkurugenzi wa afya katika kaunti hii Dkt Nobert Abuya ambaye amesema kuwa kumekuwepo na mkurupuko wa ugonjwa huo maeneo mbali mbali ya kaunti hii kwa mwaka mmoja sasa akiwataka wazazi kuwa watulivu wakisubiri chanjo hiyo.
Obuya amesema ugonjwa huo unawaathiri watoto wengi kutokana na kutokuwepo kinga thabiti mwilini hali inayosababishwa na wazazi wengi kutowapelekea wanao kupokea chanjo hiyo kwa wakati.
Amewahimiza wazazi kuhakikisha kuwa wanao wenye umri wa miezi tisa wanapata chanjo ya kwanza ya surua, na ya pili kwa watoto wenye umri wa miezi 18, wakati wanaposubiri kuanza kampeni ya kutoa chanjo hiyo kaunti hii.