CHANGAMOTO ZINAZOMKUMBA MTOTO WA KIKE POKOT MAGHARIBI ZATAJWA KUCHANGIA MATOKEO DUNI KATIKA MITIHANI YA KITAIFA.

Na Emmanuel Oyasi

Changamoto nyingi ambazo mtoto wa kike anapitia miongoni mwa jamii katika kaunti ya Pokot magharibi zimetajwa kuwa chanzo cha wengi wa wanafunzi wa kike kutofanya vyema katika mitihani yao ya kitaifa.

Naibu mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya Nasokol Dinah Mnang’at alitaja visa vya mimba za utotoni na ndoa za mapema kuwa miongoni mwa changamoto ambazo mtoto wa kike anakumbana nazo katika jamii.

Aidha Mnang’at alisema kwamba jamii nyingi katika kaunti hiyo bado hazijakumbatia elimu kwa ajili ya mtoto wa kike, hali ambayo inawafanya baadhi yao kuendeleza elimu yao kwa hofu ya kuondolewa shuleni wakati wowote, swala analosema kwamba linaathiri pakubwa kimasomo.

“Wasichana hawa wanatoka katika meeneo ambayo yametengwa, na wana changamoto nyingi sana. Ukiona msichana ambaye amejikaza hadi kumaliza shule kwenye kidato cha nne, atakuwa amjitolea sana maana wanakumbwa na changamoto tele ambazo huwafanya wengi wao kuachia masomo njiani.” Alisema Mnang’at.

Hata hivyo Mnag’at ambaye shule yake ilisajili alama ya jumla ya 5.7, mwanafunzi wa kwanza akipata alama ya A-, alisema kwamba wanaendeleza mikakati ambayo itasaidia kuhakikisha kwamba mtoto wa kike pia anapata elimu bila ya kuhofia hatma yake.

“Tunaendeleza mikakati mbali mbali ambayo itasaidia pakubwa katika kuhakikisha kwamba changamoto ambazo zinawakumba wanafunzi wa kike zinasuluhishwa, ili pia kuwapa nafasi ya kuendeleza masomo yao na kuafikia ndoto zao maishani.” Alisema.