CHANGAMOTO YATOLEWA KWA VIJANA KUHUSIKA KATIKA KUKABILI MABADILIKO YA TABIA NCHI.


Vijana kutoka wadi ya Chepareria eneo bunge la Pokot kusini wametakiwa kukumbatia upanzi wa miti na kuelimisha jamii kupitia mitandao kufuatia ongezeko la ukame unaoshuhudiwa nchini.
Mshirikishi wa shirika la Green the future program Pkiror kedii alisema kwamba kumekuwepo na mabadiliko ya tabia nchi kutokana na shughuli za kibinadam.
“Tunafanya kazi ya kuelemisha wananchi kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na tunashirikiana kwa wingi na vijana. Tunawahimiza vijana hao waweze kujishughulisha pakubwa na upanzi wa miti kama njia moja ya kuhakikisha kuwa hali ya anga inakuwa sawa.” Alisema.
Aidha amewataka vijana kujiunga na mashirika ya kiserikali pamoja na yale ya kibinafsi kwa kuanzisha mikakati ya kuelimisha jamii kuhusu mabadiliko ya tabia nchi kupitia mitandao.
“Vijana hawa wanafaa kujiunga na mashirika ya mazingira ya kiserikali na kibinafsi na kuendeleza juhudi hizo hasa kwa kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha umma kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.” Alisema.
Kedii pia aliitaka serikali ya kaunti pamoja na ya kitaifa kuweka mikakati na sheria za kuwezesha kupatika kwa fedha za kuendesha miradi ya kutunza mazingira.
“Serikali ya kitaifa pamoja na ya kaunti zinapasa kubuni mkakati utakaohakikisha kwamba kuna fedha za kutosha zitakazosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.” Alisema.