CHAMA KIPYA POKOT MAGHARIBI CHAZIDI KUPOKEA PINGAMIZI.


Juhudi za kubuniwa chama kipya cha kisiasa katika kaunti hii ya Pokot magharibi zinazoendelezwa na gavana John Lonyangapuo na mbunge wa pokot kusini David Pkosing zimeendelea kupokea pingamizi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa kaunti hii ambao wametaja chama hicho kuwa cha watu binafsi.
Wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto na mwakilishi wadi maalum Elijah Kasheusheu, viongozi hao wamedai kuwa wanaoshinikiza kubuniwa chama hicho wanaongozwa na malengo ya kibinafsi ya kupata fedha zinazotolewa kwa vyama wakisema huenda yasiafikiwe.
Moroto amewataka viongozi wa kisiasa kutoka kaunti hii pamoja na wananchi kwa ujumla kutokimbilia vyama vipya vinavyobuniwa na badala yake kujiunga na vyama vilivyopo ambavyo vitawapa nafasi ya kusikika katika ngazi za kitaifa.
Ni kauli ambayo imetiliwa mkazo na mwakilishi wadi maalum Elijah Kasheusheu ambaye amekitaja chama hicho kuwa cha kikabila na ambacho hakina nguvu zozote ikizingatiwa kuwa hakiwahusishi viongozi wakuu katika kaunti hii ya Pokot magharibi.