CHAMA CHA KUPPET POKOT MAGHARIBI CHAPONGEZA SHULE ZA KAUNTI HIYO KWA MATOKEO BORA YA MTIHANI WA KCSE.
Chama cha walimu wa shule za upili na vyuo vya kadri KUPPET tawi la kaunti ya Pokot magharibi kimepongeza matokeo bora ya mtihani wa kitaifa kwa kidato cha nne KCSE ya mwaka 2023 ambayo yalisajiliwa na shule za kaunti hiyo.
Akizungumza na wanahabari katika afisi yake katibu mkuu wa chama hicho Wilfred Kamuto alisema kwamba shule nyingi za kaunti hiyo zimefanya vyema zaidi katika mtihani huo wa mwaka jana ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2022.
Kamuto aliwapongeza walimu pamoja na wadau mbali mbali katika sekta ya elimu kaunti hiyo ya Pokot magharibi kwa ushirikiano ambao umekuwepo na kupelekea kusajiliwa matokeo bora katika mtihani wa KCSE.
“Ningependa kuwashukuru walimu wetu katika kaunti hii kwa matokeo bora ya mtihani wa kitaifa KCSE, kwa sababu kulingana na matokeo ambayo tumeendelea kupokea, shule nyingi zimefanya vyema ikilinganishwa na mwaka 2022.” Alisema Kamuto.
Wakati uo huo Kamuto alitumia fursa hiyo kuwarai wazazi katika kaunti hiyo kushirikiana na uongozi wa shule ambako wanao wanasomea kwa kutekeleza jukumu lao la kulipa karo kwa wakati huku pia akiwataka walimu wakuu kutowatuma wanafunzi nyumbani kwa ajili ya karo
Aliwahimiza walimu kuelewana na wazazi kuhusiana na ulipaji wa karo hiyo ili kuwapa nafasi wanafunzi kuendelea na masomo yao.
“Nawahimiza wazazi kutekeleza jukumu lao la kulipa karo ya wanao ili kuruhusu shughuli za masomo shuleni kuendelea bila ya kutatizika. Pia natoa wito kwa wakuu wa shule wasiwatume nyumbani kiholela wanafunzi ambao hawajakamilisha karo. Wanafaa kuelewana na wazazi kuhusu jinsi wataweza kulipia karo hiyo ili wanafunzi wapate wakati mzuri darasani.” Alisema.