CHAMA CHA KNUT POKOT MAGHARIBI CHASHUTUMU VISA VYA WAZAZI KUVAMIA SHULE KULALAMIKIA MATOKEO.

Na Emmanuel oyasi.

Chama cha walimu nchini KNUT kimeshutumu vikali visa ambapo wazazi wamevamia shule maeneo mbali mbali ya nchi kulalamikia matokeo mabaya ya mtihani wa kitaifa kwa kidato cha nne KCSE mwaka 2023.

Akizungumza baada ya kikao na walimu wakuu, katibu mkuu wa chama hicho tawi la kaunti ya Pokot magharibi Martine Sembelo alisema kwamba jukumu la kuhakikisha matokeo bora katika mitihani ya kitaifa si la walimu pekee bali la wadau wote ikiwemo walimu wazazi na hata wanafunzi.

Sembelo alisema zipo njia bora za kutumia kulalamikia matokeo mabaya ya mitihani ikiwemo kuandaa kikao na uongozi wa shule ili kubaini kilichopelekea hali hiyo, wala si kuvamia shule na kuwadhalilisha walimu mbele ya wanafunzi.

“Tunashutumu vikali visa vya wazazi kuvamia shule na kuwadhalilisha walimu mbele ya wanafunzi kwa madai kwamba shule zimefanya vibaya katika mitihani ya kitaifa. Si jukumu la walimu pekee kuhakikisha matokeo bora ya mitihani, bali ni jukumu la wadau wote hata ikiwemo wazazi.” Alisema Sembelo.

Aidha Sembelo alilalamikia kile amesema kwamba baadhi ya wafadhili wanahitilafiana na shughuli za shule mbali mbali kutokana na tofauti zao na baadhi ya walimu akisema kwamba walimu wameajiriwa na tume ya huduma za walimu TSC kufunza shule yoyote nchini.

“Kuna baadhi ya wafadhili pia ambao wanahitilafiana na uongozi wa shule. Tunawaambia wafadhili hawa kwamba walimu wameajiriwa na serikali kufunza kila shule hapa nchini. Si wafadhili wanaowaajiri walimu.” Alisema.