CHAMA CHA KNUT KAKAMEGA CHA SHUTUMU WIZARA YA ELIMU KWA UFUNGUZI WA SHULE MWAKA UJAO

KAKAMEGA


Chama cha kitaifa cha walimu KNUT tawi la Kakamega kimeelezea kutoridhishwa na matayarisho ya kufungua shule mwakani kikihofia uwezekano wa ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari katibu wa KNUT tawi la Kakamega ya kati Tom Ingolo amesema serikali inastahili kuwekeza pakubwa katika unyunyuziaji wa dawa ili kuzuia virusi vya corona shuleni na kushughulikia vyema swala la walimu wenye umri wa zaidi ya miaka hamsini na minane kusalia nyumbani.
Wakati uo huo Ingolo amesikitia ufujaji wa fedha za kukabili janga la corona licha ya kuongezeka kwa maambukizi hasa mashinani.
Hayo yakijiri chama cha walimu nchini KNUT kimetishia kuandaa mgomo wa kitaifa mwezi Januari mwaka ujao kulalamikia hatua ya tume ya kuajiri walimu nchini TSC kukihangaisha.
Katibu mkuu wa chama hicho Wilson Sossion ameshtumu wasimamizi wa TSC akisema wamekuwa wakihujumu utendakazi wa knut kwa kuwaondoa wanachama wake kutoka sajili kwa nia isiyofaa.
Katika mkao na wanahabari katika kaunti ya Bomet Sossion aidha anashinikiza tume hiyo kufanyiwa mabadiliko zaidi kuwa na uwezo wa kutekeleza wajibu wake vilivyo kupitia mabadiliko ya katiba.