CHAKULA CHA MSAADA KILICHOPOTEA KANYARKWAT CHAPATIKANA.
Siku chache tu baada ya baadhi ya viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi kulalamikia kupotea kwa chakula cha msaada eneo la Kanyarkwat na mnagei, chakula hicho sasa kinadaiwa kupatikana.
Akizungumza baada ya kikao na wakuu wa usalama ikiwemo machifu wa eneo hilo, mwakilishi wadi ya mnagei Richard Todosia alisema chakula hicho sasa kitaanza kusambazwa Jumatatu maeneo hayo ili wakazi wanaokabiliwa na makali ya njaa wapate kunufaika.
Todosia ametoa hakikisho kwa wakazi wa maeneo hayo kuwa yeye kwa ushirikiano na viongozi wengine pamoja na wadau wa usalama watahakikisha chakula kinachotolewa na serikali kwa ajili ya wakazi kinawafikia inavyohitajika.
“Kufikia sasa nimefurahi kwa sababu kuna matumaini ya chakula ambacho tulikuwa tunafuata, kwa sababu chakula hicho kimepatikana na tutaanza kupeana jumatatu kwa waliokusudiwa. Tunafurahi kwa ushirikiano wa machifu na manaibu wao pamoja wasaidizi wa makamishina ambao umepelekea kupatikana chakula hicho.” Alisema Todosia.
Wakati uo huo Todosia alitoa wito kwa wakazi wa maeneo haya na kaunti ya Pokot magharibi kwa jumla kuwa macho na kuhakikisha mipango yote ambayo inatolewa na serikali inaafikia malengo hitajika.
“Ningependa pia kutoa wito kwa kila mmoja wetu hapa mnagei, Kanyarkwat na pokot yote kwamba tuwe macho na tuchunge chochote ambacho serikali inatoa hasa chakula cha shule, na tuhakikishe kwamba kinaafikia malengo hitajika.” Alisema Todosia.