CDF KACHELIBA YAPUUZA MADAI YA KUTOKUWA NA UWAZI KATIKA MATUMIZI YA FEDHA.
Meneja wa hazina ya CDF eneo bunge la Kacheliba kaunti hii ya Pokot magharibi Wilson Koringura amepuuzilia mbali madai ya kutokuwepo uwazi katika ugavi wa fedha hizo eneo bunge hilo.
Akizungumza na kituo hiki Koringura amesema kuwa taratibu mwafaka hufuatwa kabla ya kutolewa fedha hizo ambapo zipo kamati katika wadi zote sita za eneo bunge hilo ambazo hupokezwa fedha baada ya kuwasilisha orodha ya wanafunzi wanaohitaji msaada wa basari, shughuli inayotekelzwa kwa uwazi mkubwa.
Aidha Koringura amekariri kuwa afisi yake iko makini kuhusu wanafunzi ambao wanapokezwa fedha hizo, wanafunzi kutoka jamii masikini wakipewa kipau mbele kabla ya kuzingatia wanafunzi kutoka jamii ambazo zina uwezo wa kifedha japo kila mwanafunzi hunufaika na fedha husika.
Wakati uo huo Koringura ametumia fursa hiyo kuwaeleza wanaohitaji basari kuwa kipindi cha maombi kinaendelea na tarehe ya mwisho ya kutuma maombi itakuwa tarehe 31 mwezi huu wa januari, huku akiwataka wanaotuma maombi kuyaambatanisha na kiwango cha karo wanachaodaiwa.