CBC YAUNGWA MKONO KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI

Kamati ya elimu ya kutathmini utekelezwaji wa mtaala mpya wa elimu CBC iliyoundwa na rais William Ruto kutafuta maoni kwa wakenya kuhusu utekelezwaji wa mtaala huo ikitarajiwa kuendeleza vikao hivyo kote nchini, baadhi ya wadau katika sekta ya elimu wamesifia mfumo huo.

Wakiongozwa na mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya Pserum katika kaunti hii ya Pokot magharibi Regina Chedotum wadau hao wamesema kwamba mfumo huo ni bora kutokana na hali kwamba unawahusisha zaidi wanafunzi akisisitiza ni bora utekelezwe kutokana na jinsi serikali imewekeza katika mtaala huo.

Wakati uo huo Chedotum amesema kwamba wako tayari kuwapokea wanafunzi wa gredi ya sita wanaotarajiwa kujiunga na shue za upili daraja ya chini hasa baada ya kujengwa madarasa zaidi katika shule hizo na walimu kupokea mafunzo ya kutekeleza mtaala huo.

Chedotum aidha amewahimiza wazazi kuwajibika katika jukumu lao la kuhakikisha kwamba wanawalipia wanao karo kwa wakati unaofaa ili kuwawezesha wanafunzi kusalia shuleni na kuendeleza masomo yao hasa ikizingatiwa muhula huu ni mfupi mno.