CBC YAENDELEA KUWAKANGANYA WADAU WA ELIMU.


Hisia mseto zimeendelea kuibuliwa miongoni mwa wadau katika sekta ya elimu kuhusu utekelezwaji wa mtaala mpya wa elimu CBC wakati rais William Ruto akiahidi kubuni kamati ya kutafuta maoni kuhusu utekelezwaji wa mtaala huo na kutoa mapendekezo yake mwakani.
Wakiongozwa na mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Kesogon Emmanuel Mukoe baadhi ya wadau wameelezea utayarifu wao hasa wakitaja uwepo wa madarasa ya kutosha kutekeleza mtaala huo japo wakilalamikia uhaba wa walimu wa kutosha.
“Darasa moja tayari limekamilika kwa ajili ya mtaala wa CBC na kuna mengine mawili ambayo yanaendelea kukamilika. Kwa jumla tutakuwa na madarasa matatu ambayo tulipewa na serikali. Tatizo ni kwamba hatuna walimu wa kutosha kutekeleza mtaala huo na hili linahitajika kushughulikiwa haraka iwezekanavyo.” Alisema.
Hata hivyo baadhi ya wadau wakiongozwa na mkurugenzi wa shule ya msingi ya makutano central Albert Mukhwana, wamependekeza kupewa muda wa kujiandaa kabla ya utekelezwaji kikamilifu wa mtaala huo hasa ikizingatiwa idadi ndogo ya walimu ambao wamepokea mafunzo ya kuutekeleza.
“Sidhani kwamba itawezekana kutekelezwa kikamilifua mtaala huu. Kwa mfano kuwapeleka walimu kwa mafunzo mafupi kila mara kutaleta mkanganyiko kwa wanafunzi. Tunahitaji muda kwa walimu hata kujiunga na vyuo vikuu kupokea mafunzo ya mtaala huo na baada ya miaka miwili walimu watakuwa wamejiandaa vyema kuutekeleza.” Alisema.
Akizungumza jumanne wiki hii baada ya kuapishwa rasmi, rais William Ruto aliahidi kubuni kamati ambayo itakusanya maoni kutoka kwa wakenya kuhusu utekelezwaji wa mtaala huo kabla ya kutoa mwelekeo kuhusu hatma ya masomo ya CBC nchini.
Ikumbukwe wakenya wa matabaka mbali mbali wamekuwa wakilalamikia utekelezwaji wa mtaala huo wakisema kuwa ni ghali mno kwa wazazi.