CALEB AMISI APIGWA JEKI KUWANIA TENA UBUNGE SABOTI, TRANS NZOIA.


Mbunge Saboti Caleb Amisi amepigwa jeki katika azma yake ya kuwania tena ubunge wa eneo bunge hilo katika uchaguzi mkuu ujao baada ya mgombea wa kiti hicho kwa chama cha ODM kwenye uchaguzi mkuu uliopita Askofu Robert Makona kutangaza rasmi kumuunga mkono Amisi kwenye uchaguzi wa mwe zi agosti.
Akihutubu kwenye hafla moja eneo bunge hilo, Askofu Makona amesema ana imani na uongozi wa mbunge wa sasa kwa kile amesema kuwa ni kiongozi mwenye agenda ya maendeleo kwa wenyeji mbali na kuzingatia amani na umoja wa jamii zote za eneo hilo.
Kauli yake imeungwa mkono na aliyekuwa waziri wa fedha katika Kaunti ya Trans nzoia Ken Simiyu, ambaye amesema Amisi ameimarisha elimu kupitia ujenzi wa miundo msingi katika taasisi za elimu mbali na kuanzisha miradi ya kukwamua wenyeji kutoka katika umaskini sehemu zote eneo bunge hilo.