BWENI LA SHULE YA UPILI YA WAVULANA YA GOSETA IMETEKETEA


Shule ya upili ya wavulana ya Goseta kwenye kaunti ya Trans Nzoia imekuwa ya hivi punde kuteketea usiku wa kuamkia leo huku wazima moto kwa ushirikiano na wananchi wakifanikiwa kuuzima moto huo ambao ulikuwa umeteketeza bweni hilo lote.
Naibu mkuu wa idara ya wazima moto Richard Wafula amesema kuwa moto huo ulianza mwendo wa saa mbili usiku na kusambaa kwa mwendo wa kasi kwa kuwa ni jengo la mabati wanafunzi walipokuwa darasani.
Chanzo cha moto huo hata hivyo haijulikani huku uchunguzi ukianzishwa.
Hata hivyo wataalam wa maswala ya akili nchini wamesema kuwa ipo haja ya wanafunzi wote nchini kufanyiwa vipimo ili kubainisha iwapo wanatumia au wamewahi kutumia dawa za kulevya.
Rose Wachira ambaye ni mmoja wa wataalam wa maswala ya akili nchini katika kituo cha Extra Mile Guidance and Canceling wameishauri wizara ya elimu kufanya hivyo akisema kuwa wanafunzi wengi walijihusisha na utumiaji wa dawa hizo walipokuwa nyumbani kwa likizo ndefu iliyosababishwa na janga la korona.