BUNGE LA TRANS NZOIA LATAKIWA KUMAKINIKA KATIKA KUWAPIGA MSASA MAWAZIRI WA NATEMBEYA.

Gavana wa kaunti ya Trans nzoia George Natembeya ametetea orodha ya majina ya maafisa watakaohudumu katika serikali yake na ambayo anatarajiwa kuwasilisha katika bunge la kaunti hiyo kupigwa msasa akisema watawajibikia kikamilifu kazi zao.

Gavana Natembeya alisema kuwa alizingatia umakinifu katika kuteua maafisa hao anaosema kwamba wana tajriba ya kutosha kuhudumu katika nyadhifa watakazoteuliwa akiwaomba wabunge katika bunge hilo kuunga mkono orodha hiyo.

“Watu ambao nitaleta mbele ya bunge la kaunti kupigwa msasa ni watu ninaojua kwamba wako tayari kuwahudumia watu wetu na wafunge mabao ya kuondoa umasikini, walete kazi katika kaunti hii ili watu wetu waanze kutembea kwa heshima.” Alisema Natembeya.

Natembeya aliongeza kwa kusema, “Tafadhali spika na wabunge sitaki nianze kusema kwamba nimeshindwa kufanya kazi kwa sababu niliwaletea hawa na mkawakataa, hapana, wacha tutembee katika njia moja kwa ajili ya wananchi.”

Wakati uo huo Natembeya aliwataka wakazi wa kaunti hiyo kutowatazama maafisa hao kulingana na maeneo wanakotoka bali kulingana na uwezo wao wa kutekeleza majukumu watakayokabidhiwa katika serikali ya kaunti hiyo.

“Kuna watu wetu ambao wanapenda sana kutazama ligi ya Premier. Ikifika wikendi unakuta wengine wanasema wako Chelsea, wengine Arsenal, wengine Manchester United na hata wengine wanataka kupigana kama timu yake imepoteza. Ningependa mtazame hizo timu iwapo wanazingatia ujuzi wa wachezaji au mahali anakotoka.” Alisema Natembeya.

[wp_radio_player]