BUNGE LA POKOT MAGHARIBI LASITISHA SHUGHULI KULALAMIKIA MISHAHARA.

Bunge la kaunti hii ya Pokot magharibi ni la hivi punde kusitisha shughuli zake wabunge katika bunge hilo wakishinikiza tume ya kuratibu mishahara ya wafanyikazi SRC kusitisha hatua ya kupunguza mishahara yao.

Wakiongozwa na kiongozi wa wengi Martine Komongiro, wabunge katika bunge hilo walisema kwamba wamelazimika kuchukua hatua hiyo ili kuwa katika mkondo mmoja na wenzao kutoka kaunti zingine hasa baada ya kukamilika makataa waliyotoa kwa tume ya SRC kuongeza mishahara yao.

“Kama wabunge katika bunge la kaunti tumeamua kutembea pamoja na wenzetu katika kaunti zingine, kusitisha shughuli za bunge hadi pale tume ya kuratibu mishahara SRC itakapotusikiliza na kufanya kile tunachoshinikiza.” Walisema.

Viongozi hao walisema licha ya kwamba ndio wanaobeba mzigo mkubwa wa kuwahudumia wananchi ikizingatiwa ndio walio karibu na mwananchi, wanapokea mishahara ya chini mno ikilinganishwa na maafisa wengine wa serikali.

“Hatutarajii chochote ila kutendewa haki. Inasikitisha kuona maafisa wengine wa serikali wakipokea mishahara minono huku sisi tukifinyiliwa wakati ambapo ni waakilishi wadi walio na mzigo mzito wa kuwahudumia wananchi ikizingatiwa ni sisi ndio tulio karibu na mwananchi.” Walisema.

Walitoa wito kwa rais William Ruto kuingilia kati swala hilo na kuishauri tume ya mishahara SRC kuangazia upya uamuzi wake, wakiapa kutorejelea shughuli za bunge hadi matakwa yao yatakapotekelezwa kikamilifu.

Tunatoa wito kwa rais William Ruto kuingilia kati na kuishauri tume ya SRC kutafakari upya kuhusiana na uamuzi wake wa kupunguza mishahara yetu. Sisi hatutarudi bungeni hadi tupokee haki yetu.” Walisema.