BUNGE LA POKOT MAGHARIBI LAREJELEA VIKAO BAADA YA KUSITISHWA KWA MUDA KULALAMIKIA MISHAHARA.

Bunge la kaunti ya Pokot magharibi limerejelea rasmi vikao vyake baada ya kusitisha vikao hivyo kwa muda, wabunge katika bunge hilo wakilalamikia maswala mbali mbali ambayo wanashinikiza serikali kutekeleza ikiwemo nyongeza ya mishahara na marupurupu.

Akizungumza na wanahabari katika majengo ya bunge spika wa bunge hilo Fredrick Kaptui alisema kwamba wamelazimika kurejelea vikao hivyo ili kushughulikia maswala mbali mbali waliyokuwa wakishughulikia kabla ya kusitisha vikao.

Kaptui alisema licha kwamba malengo yao hayajaafikiwa wana imani kwamba rais William Ruto ataweza kuyashughilikia kulingana na mpangilio wake baada ya kuonyesha nia ya kufanya hivyo.

“Tulisitisha vikao vya bunge ili kuungana na wenzetu maeneo mengine ya nchi kushinikiza maswala mbali mbali yanayotuhusu. Sasa umefika wakati wetu wa kuendelea na vikao kwa sababu kuna mambo mengi ambayo yanatusubiri kushughulikia. Japo matakwa yetu hayajaangaziwa kikamilifu,tuna imani kwamba maswala haya yatazingatiwa baada ya rais kuonyesha nia.” Alisema Kaptui.

Kauli yake ilisisitizwa na kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti hiyo Martine Komongiro ambaye alisema mazungumzo yanaendelezwa na tume ya kuratibu mishahara SRC kuhakikisha kwamba mishahara ya waakilishi wadi inaangaziwa.

Aidha Komongiro alisema hatua ya kurejelea vikao haiashirii kwamba hawapo kwenye mkondo mmoja na wenzao maeneo mengine ya nchi, akisisitiza malengo yao yangali mamoja kote nchini.

“Kuna mazungumzo ambayo yanaendelea kati ya uongozi wa muungano wa waakilishi wadi na tume ya mishahara SRC, na tuna imani kwamba yatazaa matunda. Kurejelea vikao haimaanishi kwamba tunatofautiana na wenzetu bali bado tupo pamoja katika kushinikiza matakwa ya waakilishi wadi.” Alisema Komongiro.

Zaidi ya mabunge ya kaunti 18 yalisitisha vikao kuanzia mwezi mei kulalamikia hatua ya tume ya kuratibu mishahara ya wafanyikazi wa umma SRC kupunguza mishahara yao pamoja na kuondolewa marupuru ya vikao vya bunge.