BUNGE LA POKOT MAGHARIBI LAAHIDI KUIWAJIBISHA SERIKALI BILA KUZINGATIA MIEGEMEO YA KISIASA.


Bunge la kaunti hii ya Pokot magharibi litatumia fursa hii ambapo kuna umoja miongoni mwa wabunge katika bunge hilo kuhakikisha kwamba serikali iliyo mamlakani inawajibika inavyostahili kwa ajili ya wakazi.
Haya ni kwa mujibu wa naibu spika wa bunge hilo Victor Siywat ambaye aidha alisema kwamba umoja na utulivu unaoshuhudiwa sasa umefanya rahisi kuendelezwa shughuli katika bunge hilo ikiwemo zoezi la hivi karibuni la kupasisha majina ya mawaziri walioteuliwa kuhuduma chini ya serikali ya gavana Simon Kachapin.
Siywat pia alisema kuwa anatarajia hali hiyo kushuhudiwa tena katika kupiga msasa na kuidhinisha makatibu katika wizara mbali mbali ambao wanasubiriwa kukabidhiwa na gavana Kachapin kwa ushirikiano na bodi ya huduma za umma.
“Kwa sasa bunge la kaunti lina utulivu wa kutosha. Hatuma migogoro ambayo ilishuhudiwa katika mabunge yaliyotangulia. Tumepitisha mawaziri juma moja lililopita na sasa tunangoja bodi ya huduma za umma itupe makatibu ambao tutawapiga msasa bila upendeleo na kuhakikisha wana uadilifu.” Alisema Siywat.
Wakati uo huo Siywat alisema kwamba bunge hilo linatarajiwa kuanza misururu ya mikutano kuangazia mipangilio ya serikali kutekeleza miradi mbali mbali, ili kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba miradi hiyo inakamilishwa kabla ya mwaka 2027.
“Kwa sasa tunapanga misururu ya mikutano kuhakikisha kwamba kazi zote ambazo serikali ya kaunti hii inatarajia kufanya zinakamilika kabla ya mwaka 2027.” Alisema