Bunge la kaunti ya Pokot Magharibi lapitisha sheria itakayoruhusu kuachiliwa fedha za basari

Na Benson Aswani,
Kwa muda mrefu fedha za basari katika kaunti ya Pokot magharibi zimekuwa zikitolewa kwa wanafunzi bila ya sheria rasmi ya kuongoza jinsi fedha hizo zinatolewa.
Ni kutokana na hilo ambapo bunge la kaunti hiyo lililazimika kuandaa kikao maalum alhamisi ili kupitisha sheria hiyo na kuiainisha na ile ya serikali ya kitaifa ili kutoa mwongozo wa jinsi fedha hizo zinapasa kupeanwa.
“Tumekuwa na kikao rasmi kuangalia sheria ambayo itaainisha sheria ya serikali kuu na ya kaunti kuangazia basari. Kwa muda mrefu hatujakuwa na sheria hiyo ambayo inaelekeza jinsi basari zinapasa kupeanwa,” alisema naibu spika wa bunge la kaunti Victor Siywat.
Siywat alisema sheria hiyo itaanza kutumika rasmi juma lijalo baada ya kutiwa saini na gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin ili kupisha nafasi ya fedha za basari kutumwa katika kaunti hiyo na serikali kuzisambaza kwa shule mbali mbali.
“Kuanzia wiki ijayo sasa serikali ya kaunti itapata muda wa kutumia hiyo sheria kuagiza pesa kutoka serikali kuu, kwa sababu tayari tumeweka fedha hizo kwenye bajeti na lililosalia ni kuagiza tu kutoka hazina kuu ili zije kwa akaunti ya kaunti,” alisema.
Siywat alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa viongozi wa kisiasa kaunti ya Pokot magharibi kutoingiza siasa kwenye maswala ya elimu na badala yake kuunga mkono mipango ya serikali ambayo inanuiwa kuwafaa wanafunzi.
“Nawahimiza viongozi wetu wote kwamba inapofika kuhusu maswala ya elimu ya watoto wetu tuweke siasa kando, tushikane wote na tuunge mkono mipango ya serikali bila kuwepo na tofauti za mirengo,” alisema.
Kumekuwepo na mivutano baina ya gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin na seneta Julius Murgor kuhusu kuzuiliwa pesa hizo na mdhibiti wa bajeti, seneta akilaumiwa kwa madai ya kutoa kauli kwenye bunge la seneti ambayo ililazimu kamati ya bunge hilo kuandikia mdhibiti wa bajeti kuzizuia.