BOWEN: OPARESHENI YA USALAMA IMEFANIKIWA BONDE LA KERIO.
Idara ya usalama eneo la pokot kusini katika kaunti ya Pokot magharibi imeelezea kufanikiwa oparesheni ya kiusalama ambayo inaendeshwa na maafisa wa polisi kwa ushirikiano na wale wa KDF hasa maeneo ya mipakani.
Naibu kamishina eneo hilo David Bowen alisema kwamba ikilinganishwa na miaka ya awali, tangu kuanza kwa oparesheni hiyo hali ya usalama imeanza kushuhudiwa maeneo hayo na sasa wakazi wanaishi katika maboma yao bila ya wasi wasi wa kuvamiwa na wahalifu.
Hata hivyo Bowen alielezea changamoto ya barabara na mtandao maeneo hayo, japo akiwahakikishia wakazi kwamba serikali inashughulikia hali hiyo na kwamba swala la utovu wa usalama litakabiliwa kabisa wakati changamoto hizo zitakuwa zimeshughulikiwa.
“Oparesheni ambayo inaendelezwa maeneo ya mipakani pa kaunti hii na ambayo yamekuwa yakikabiliwa na utovu wa usalama kwa muda imefaulu pakubwa. Japo sitasema kwamba tumeweza kuwakabili kabisa wahalifu, lakini ikilinganishwa na miaka ya awali visa vya uvamizi vimepungua kwa kiwango kikubwa.” Alisema Bowen.
Wakati uo huo Bowen alipongeza ushirikiano ambao umekuwepo baina ya idara ya usalama na serikali ya kaunti pamoja na wananchi kwa ujumla ambao amesema kwamba umesaidia pakubwa katika juhudi za kuhakikisha usalama unaafikiwa maeneo hayo ya mipakani.
“Ushirikiano ambao umekuwepo kati ya serikali ya kaunti hii, maafisa wetu wa polisi, na wananchi umesaidia pakubwa kuhakikisha kwamba visa vya uvamizi vinapungua.” Alisema.