BISAU AJIONDOA KWENYE KINYANG’ANYIRO CHA UGAVANA TRANS NZOIA NA KUMUUNGA MKONO NATEMBEYA.


Katibu wa miundo msingi katika afisi ya naibu rais Willaim Ruto Kakai Bisau amejiondoa katika kinyang’anyiro cha ugavana kaunti ya Trans nzoia na badala yake kutangaza kuwania kiti cha ubunge eneo bunge la Kiminini.
Bisau ambaye alilenga awali kuwania ugavana kupitia chama cha UDA ametangaza kumuunga mkono mgombea wa DAP-K George Natembeya kwenye azma yake ya kumrithi gavana anayeondoka Patrick Khaemba.
Akizungumza baada ya kupokelewa rasmi hiyo jana katika chama cha DAP-K katika makao makuu ya chama hicho jijini Nairobi Bisau amekariri kauli yake kuwa alikihama chama cha UDA baada ya kubaini kwamba chama hicho kitamuunga mkono mwaniaji wa ugavana wa chama cha ford Kenya Chris Wamalwa.
Wakati uo huo Bisau amekosoa kauli mbiu na ajenda za muungano wa kenya kwanza unaoongozwa na naibu rais William Ruto akisema kwamba hazitawafaa wananchi wa kawaida na ni mbinu za viongozi wanaoegemea muungano huo kusaka uungwaji mkono wa wakenya.