BIASHARA YA MAKAA YAKABILIWA POKOT MAGHARIBI.

Biashara ya kuuza makaa.

Na Benson Aswani.

Afisa mkuu katika wizara ya maji, mazingira, mali asili na tabia nchi kaunti ya Pokot magharibi Leonard Kamsait amewapongeza wafanyibiashara wanaoendesha biashara ya kuuza makaa kwa kukumbatia agizo la kupiga marufuku biashara ya makaa kaunti hiyo.

Kamsait alisema kwamba uchunguzi ambao uliendeshwa na maafisa kutoka wizara hiyo ulibaini kwamba asilimia 80 ya wafanyibiashara wa makaa wamekumbatia agizo hilo, lililoanza kutekelezwa tarehe 23 mwezi januari mwaka huu.

“Nawapongeza wafanyibiashara wa makaa kwa kuzingatia agizo tulilotoa la kupiga marufuku biashara ya makaa kwa sababu kufikia sasa ni asilimia 80 ya wafanyibishara hao ambao wamezingatia agizo hilo. Tunataka tulinde mazingira yetu kutokana na hatua hii.” Alisema Kamsait.

Aidha alisema wafanyibiashara wachache ambao bado wanaendesha biashara hiyo hasa mjini Makutano walipewa muda hadi kufikia jana jumapili baada ya kuomba muda huo, ili kukamilisha makaa ambayo walikuwa wameagiza kabla ya kuanza kutekelezwa agizo hilo.

“Maafisa wetu walitembea mjini Makutano na kubaini kwamba wafanyibiashara ambao walikuwa wameomba muda hadi jana jumapili walikuwa wamekamilisha kuuza makaa na kufunga sehemu ambazo walikuwa wanayahifadhi.” Alisema.

Wakati uo huo Kamsait aliweka wazi kwamba wataruhusu tu makaa yanayosafirishwa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, ambayo ni magunia matatu kwa gari huku pikipiki zikiruhusiwa kubeba gunia moja, akiwataka wakazi wa kaunti hiyo kutunza miti iliyo mashambani mwao na kutoikata kiholela kwa ajili ya uchomaji makaa.

“Tunaomba wakazi watunze miti iliyo kwenye mashamba yao na kutoikata ovyo ovyo kwa ajili ya uchomaji makaa. Hatujapiga marufuku usafirishaji wa makaa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, ila usafirishaji kwa ajili ya biashara.” Alisema.