BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA YARIPOTIWA KUKITHIRI KACHELIBA WAATHIRIWA WAKUU WAKIWA VIJANA.
Wakazi eneo la Kacheliba katika kaunti ya Pokot magharibi wamelalamikia kukithiri utumizi wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana hali ambayo inatishia usalama wa eneo hilo.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa vijana eneo hilo Job Wanjala, wakazi hao aidha walidai kwamba visa hivyo vimekithiri kutokana na hali kuwa wanaokamatwa kwa kuhusika biashara hiyo wanaachiliwa huru muda mfupi baadaye bila hatua zozote kuchukuliwa dhidi yao.
Wakazi hao sasa wanamtaka OCS wa Kacheliba kwa ushirikiano na machifu kuhakikisha kwamba wanaoendeleza biashara hiyo wanakabiliwa ili kuokoa kizazi kijacho.
“Biashara ya dawa za kulevya imekithiri eneo hili la kacheliba. Vijana wamezama katika uvutaji bangi ambapo sasa wengi wao wameanza kuwa hatari kwa jamii ambapo wanawapiga wazazi wao. Na hii biashara imekithiri eneo hili kwa sababu wahusika wanaposhikwa na polisi wanaachiliwa muda mfupi baadaye kwa kupeana hongo.” Alisema Wanjala.
Akithibitisha haya OCS wa Kacheliba Tom Nyanaro alisema kwamba tayari washukiwa wawili wa biashara hiyo wamekamatwa na kufikishwa mahakamani, na kwamba wanaendelea kufuatilia habari wanazopokea akiahidi kuhakikisha kwamba biashara hiyo inakomeshwa.
Mmoja wa wanaosambaza bangi alikamatwa akitokea njia ya makutano na tukamfikisha kotini. Tuna habari kwamba kuna wale ambao wanaletewa bangi na kuuza eneo hili na tunaendelea kuwaandama. Wakati ukifika tutawakamata na kuhakikisha kwamba biashara hii inaisha kabisa Kacheliba.” Alisema Nyanaro.