BENKI YA KCB YAANZISHA MCHAKATO WA KUWATAMBUA WANAFUNZI WATAKAOFADHILIWA.
Benki ya KCB tawi la Kapenguria kaunti hii ya Pokot magharibi imeanzisha mchakato wa kuwatambua wanafunzi werevu kutoka jamii masikini waliofanya mtihani wa kitaifa kwa darasa la nane KCPE na ambao watafadhiliwa na wakfu wa benki hiyo katika masomo yao ya shule za upili.
Akizungumza na wanahabari baada ya kuzindua mchakato huo meneja wa benki hiyo Paul Mutai amesema kuwa wanalenga wanafunzi 20 wenye mahitaji zaidi idadi hii ikiwa imeongezeka kutoka wanafunzi watano ambao benki hiyo imekuwa ikifadhili katika miaka ya awali wakikabiliwa na kibarua cha kuwatambua wanafunzi hao kwani wamepokea maombi zaidi ya 100 ya wanaohitaji ufadhili huo.
Amesema kuwa wanafunzi wa kike ambao ni waathiriwa wa dhuluma za kijinsia kama vile ukeketaji na wale waliotoroka makwao kutokana na ndoa za mapema na hata wale waliojifungua na wanataka kuendelea na masomo watapewa kipau mbele katika mchakato huo.
Afisa katika wakfu huo Ashaka Sidi amesema wanafunzi hao watafadhiliwa hadi vyuo vikuu kwa wale watakaofanikiwa kuendeleza masomo hayo na kwamba kando na kuwalipia wanafunzi hao karo ya shule benki hiyo pia itawapa fedha za matumizi.