BENKI YA EQUITY YAZINDUA UFADHILI WA WANAFUNZI KUPITIA ELIMU SCHOLARSHIP POKOT MAGHARIBI.


Benki ya Equity tawi la Kapenguria katika kaunti hii ya Pokot Magharibi imezindua rasmi mpango wa elimu scholarship kuwafadhili wanafunzi waliofanya vyema katika mtihani wa kitaifa kwa darasa la nane KCPE na wanaotoka katika familia masikini.
Kulingana na meneja wa benki hiyo ya Equity tawi la Kapenguria James Tanui Biwott jumla ya wanafunzi 36 walifanikiwa kuteuliwa kunufaika na ufadhilii huo kati ya maombi 287 yaliyotumwa miongoni mwao wakiwa wasichana 19 huku wavulana wakiwa 17.
Hata hivyo biwott aliwahimiza wazazi wa wanafunzi waliofanikiwa kupata ufadhili huo kuendelea kuwa karibu na wanao na kutekeleza kikamilifu majukumu yao ya uzazi.

“Tulipokea maombi 297 na tukawaorodhesha wanafunzi 193 kwa ajili ya mahojiano. Wale ambao walifaulu ni wanafunzi 36 ikiwa ni pamoja na wasichana 19 huku wavulana wakiwa 17. Nawahimiza tu wazazi kuendelea kutekeleza majukumu yao ya ulezi. Wasiwaachilie sasa eti kwa sababu benki imewafadhili.” Alisema Biwott.

Ni kauli ambayo ilisisitizwa na waziri wa elimu katika kaunti hyo Rebecca Lotuliatum ambaye aidha alipongeza benki ya Equity kwa kuwafadhili wanafunzi hao, huku akiwahimiza waliofanikiwa kuteuliwa katika ufadhili huo kuzingatia kikamilifu masomo yao.

“Naishukuru sana benki ya Equity kwa kuwazia kuwasaidia watoto wetu. Kama waziri wa elimu kaunti hii nawahimiza wanafunzi ambao wamenafasika kupata ufadhili huu kutia bidii wanapofika shuleni ili waweze kuinua jina la kaunti yatu. Wazazi pia tuwape mwelekeo mwema watoto wetu.” Alisema Lotuliatum.

Baadhi ya wanafunzi ambao walinufaika na ufadhili huo walielezea furaha yao huku wakiahidi kutumia vyema muda wao masomoni kama njia moja ya kurudisha shukrani kwa benki ya Equity kwa kuwapa tumaini la maisha yao ya baadaye.

“Naishukuru sana Equity kwa kutufadhili. Sisi hatujiwezi na kama si hao ndoto zetu maishani zingedidimia. Tunaahidi kufanya bidii ili wakuu wa benki hiyo pia waone kwamba ilistahili kwao kutufadhili.” Walisema.