BARAZA LA WAZEE POKOT MAGHARIBI LAPONGEZA KUACHILIWA MIFUGO WALIOKUWA WAMEZUILIWA UGANDA.

Mwenyekiti wa baraza la wazee eneo la pokot kusini kaunti ya Pokot magharibi Mastayit Lokales amepongeza hatua ya maafisa wa polisi wa taifa jirani la Uganda kuwaachilia mifugo wa wakazi wa kaunti hiyo ambao walikuwa wameshikiliwa nchini humo.

Lokales alisema kwamba hatua hiyo ya maafisa wa polisi wa Uganda ni mfano bora kwa maafisa wa taifa hili anaodai kwamba wamekuwa kero kwa wananchi badala ya kuwahakikishia usalama wao na wa mali zao.

Lokales alisema ni kinaya kwamba maafisa kutoka taifa jirani wanajali zaidi maslahi ya wananchi wa kaunti hii kuliko maafisa wa taifa hili hasa wanaoendesha oparesheni ya kuwakabili wahalifu ambao wamesababisha utovu wa usalama maeneo ya mipakani pa kaunti hiyo.

“Tunashukuru sana maafisa wa usalama katika taifa la Uganda kwa kuwaachilia mifugo wa wakazi wa Pokot. Tunafurahi sana kwa sababu ng’ombe wote wa wapokot ambao walikuwa wanaishi Uganda wamerejeshwa nyumbani.” alisema Lokales.

Wakati uo huo Lokales alitoa wito kwa idara ya usalama katika taifa hilo la Uganda kuwaruhusu wakazi wa jamii ya Pokot kulisha mifugo wao kwenye ardhi ya taifa hilo ikizingatiwa hali ya ukame ambayo inashuhudiwa maeneo mengi ya kaunti hiyo.

“Sasa hao ng’ombe ambao wamerejea hawana pahali pa kulishwa. Naomba idara ya usalama katika taifa la Uganda kuwaruhusu wafugaji wetu kulisha mifugo katika taifa hilo kwa sababu maeneo mengi ya kaunti hii yanakabiliwa na ukame na hakuna lishe kwa mifugo.” Alisema.