BARAZA LA WAZEE POKOT MAGHARIBI LAENDELEZA MIKAKATI YA KUBUNI SHERIA ZA KUKABILI UKEKETAJI.
Harakati za kukabiliana na utamaduni wa ukeketaji katika kaunti ya pokot magharibi zimepigwa jeki baada ya baraza la wazee wa jamii ya pokot, kuahidi kuhusika katika vita dhidi ya mila hiyo.
Baraza hilo kupitia viongizi wake tayari limechapisha sheria zinazoelezea tamaduni zinazofaa, zile zisizostahili kutekelezwa na adhabu itakayotolewa kwa watakaopatikana wakiendeleza mila zilizopitwa na wakati.
Naibu katibu wa baraza hilo phillip lomongin alisema kwamba nakala ya sheria hiyo itawasilishwa kwa wizara ya utamaduni, kisha ipelekwe kwenye baraza la mawaziri, na bunge la kaunti ili kupasishwa baada ya wananchi kutoa maoni yao.
“Sheria hizi zinanuia kuhakikisha kwamba tunalinda hadhi ya mtoto wa kike katika jamii, ambaye kwa miaka mingi amekuwa mwathiriwa mkuu wa tamaduni zilizopitwa na wakati. Tunahitaji kuhamasisha umma kupitia sheria hizi ili kuhakikisha tamaduni hizi zinatokomezwa kabisa.” Alisema Lomongin.
Nao wanachama wa baraza hilo wakiongozwa na william lepetakou walisema kuwa sheria hizo pia zitapendekeza adhabu kwa wanaume wanaowapachika mimba wanafunzi na pia jinsi ya kukabili dhuluma za kijinsia.
“Visa vya mimba za mapema vipo juu sana eneo hili kwa sababu hamna mikakati ambayo imewekwa kuzuia tabia hii. Sheria ambazo tunatarajia kuweka zitakuwa kali sana ambapo mtu hataweza kufikiria kumpachika mimba mtoto wa mtu.” Walisema.