BAADHI YA WANAFUNZI WAKOSA KURIPOTI KATIKA SHULE ZA UPILI POKOT MAGHARIBI LICHA YA MPITO WA ASILIMIA 100.

Na Emmanuel Oyasi.
Baadhi ya wanafunzi eneo la Weiwei pokot ya kati katika kaunti ya Pokot magharibi hawajaripoti katika shule za upili ambazo waliitwa licha ya juhudi za serikali kuhakikisha kwamba wanafunzi wote waliofanya mtihani wa darasa la nane KCPE mwaka jana wanajiunga na shule za upili.
Haya ni kwa mujibu wa naibu chifu kata ndogo ya Tokou eneo la Weiwei Filomena Karotich ambaye alitaja hali ya ukame ambao umepelekea wengi wa wazazi kuishi katika hali ya umasikini kuwa chanzo cha hali hiyo.
Karotich alisema kwamba wengi wa wazazi eneo hilo wanategemea shughuli ya kutafuta dhahabu ambayo haitoshelezi mahitaji yao, ikizingatiwa kwa sasa bei ya mifugo iko chini sana kutokana na ukosefu wa lishe ambao umesababishwa na ukame.
“Baadhi ya wazazi hawajakuwa katika nafasi ya kuwapeleka wanao katika shule za upili licha ya wao kufanya vyema katika mtihani wa kitaifa. Wazazi wengi hapa wanategemea biashara ya dhahabu ambayo haitoshelezi hata mahitaji yao pale nyumbani.” Alisema Karotich.
Hata hivyo alisema kwamba kama wakuu wa utawala wanafanya kila juhudi kuhakikisha wakazi wengi wanakumbatia elimu kwa kutoa uhamasisho kwa wazazi kuhusu umuhimu wa elimu kwa wanao.
“Tunaendelea kuwahimiza wazazi maeneo haya kuhusu umuhimu wa masomo kwa ajili ya wanao. Tunakutana nao na kuwapa moyo kukumbatia elimu kwa sababu tunajua kwamba kuna manufaa makubwa kwa wao kupata elimu.” Alisema.