BAADHI YA WAFANYIKAZI WA KAUNTI POKOT MAGHARIBI WALALAMIKIA KUSITISHWA MISHAHARA YAO.

Baadhi ya wafanyikazi wa serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi wamelalamikia kupitia hali ngumu wakidai kutolipwa mishahara licha ya kutoa huduma.

Wakizungumza na wanahabari wafanyikazi hao walisema tangu kuajiriwa mwezi februari mwaka huu hawajalipwa fedha zozote wengine wakilipwa mwezi mmoja pekee.

Walisema kwamba licha ya juhudi zao kupata majibu kutoka kwa idara mbali mbali za serikali kuhusiana na hali yao hamna lolote ambalo limeafikiwa hadi kufikia sasa.

“Licha ya kuajiriwa na serikali mwezi februari mwaka huu, wafanyikazi ambao waliajiriwa wakati huo hawajakuwa wakilipwa mshahara wao. Kuna wale ambao wamepata mshahara wa mwezi mmoja tu na kuna wale ambao wamemaliza miezi minane bila ya kulipwa licha ya kuwa kazi.” Walisema.

Waliongeza kwa kusema kwamba, “Tumejaribu kuwasiliana na idara mbali mbali za serikali ya kaunti ili watueleze ni kwa nini mishahara yetu imesimamishwa ila hatujapata majibu.”

Wafanyikazi hao walipuuzilia mbali madai kuwa waliajiriwa kwa misingi ya kisiasa, wakisisitiza kwamba waliajiriwa kwa kufuata sheria wakiitaka serikali ya kaunti hiyo kutimiza matakwa ya kisheria na kuwalipa fedha zao.

“Si vyema kwa mtu kufanya kazi, wakati huo ana majukumu ya kifamilia, hata wengine wametoka maeneo mengine kuja eneo hili kwa ajili ya kazi na hawalipwi. Na haya madai kwamba ajira zetu zilichangiwa kisiasa ni porojo tupu. Sheria ilifuatwa katika mchakato mzima wa kutupa ajira.” Walisema.